Utangulizi: Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu leo (Jumapili, Oktoba 20, 2024) imetangaza Awamu ya Tatu (Batch Three) yenye wanafunzi 19,345 wa shahada ya awali waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 59.49 bilioni kwa mwaka wa masomo 2024/2025. Wanafunzi hawa 19,345 ni wapya wa mwaka wa kwanza wanaojiunga na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo nchini kwa ajili ya masomo ya shahada za awali (Bachelor Degrees).
Idadi ya wanafunzi wa shahada ya awali waliopangiwa yafikia 70,990
Kufuatia kutangazwa kwa Awamu ya Tatu, jumla ya wanafunzi wapya wa shahada za awali waliopangiwa mikopo imefikia 70,990 na thamani ya mikopo yao ni TZS 223.3 bilioni, wanafunzi wa kiume ni 40,164 (56.58%) na wa kike ni 30,825 (43.42%).
Mikopo kwa Stashahada
Aidha, katika awamu hii pia, wamo wanafunzi wapya wa stashahada 425 (wa mwaka wa kwanza 378 na wanaoendelea na masomo 47) ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 1.1 bilioni.
Ruzuku ya ‘Samia Scholarship’
Akisema, Mpaka sasa, jumla ya kiasi cha TZS 3.02 bilioni kimetolewa kwa ajili ya ruzuku kwa wanafunzi 599; (588 awamu ya kwanza na 11 awamu ya pili) wa mwaka wa kwanza wanaonufaika na ‘Samia Scholarship’ kwa mwaka wa masomo 2024/2025.