Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linawataarifu umma kuwa matokeo ya uhakiki wa waombaji waliochaguliwa kujiunga na masomo kwa mkupuo wa Machi, 2025 katika ngazi ya Astashahada na Stashahada yametolewa rasmi tarehe 2 Aprili, 2025.
Jumla ya waombaji 10,684 (Wanawake 5,325 – 49.8%, Wanaume 5,359 – 50.2%) waliwasilishwa kwa ajili ya uhakiki kutoka vyuo vilivyokidhi vigezo vya kudahili katika mkupuo huu. Kati yao, waombaji 10,419 (98%) (Wanawake 5,197, Wanaume 5,222) walikuwa na sifa za kujiunga na programu walizoomba, huku waombaji 265 (2%) wakikosa sifa za programu walizoomba.
Waombaji wote walioomba kujiunga na programu mbalimbali wanaweza kupata taarifa zao za uhakiki kwa kutumia misimbo iliyotumwa kwenye namba zao za simu kwa kubonyeza kitufe cha “Angalia Hali ya Uhakiki wa muhula wa Machi 2025/2026” au “Uhakiki mkupuo wa Machi, 2025/2026” kwenye tovuti ya Baraza nactvet.go.tz.
Baraza linawasisitiza waombaji wote kutunza misimbo watakayotumiwa kwani ndiyo itatumika katika udahili mara watakapofika vyuoni.
Baraza pia linavielekeza vyuo kuwasajili wanafunzi wenye sifa na watakaowasili vyuoni kwa ajili ya kuanza masomo kuanzia tarehe 7 Aprili, 2025, kwa kutumia misimbo itakayotumwa na Baraza kwenye namba za simu za waombaji. Hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya chuo kitakachokiuka taratibu za udahili.
Aidha, vyuo vimepewa nafasi ya kurekebisha na kuwasilisha taarifa za waombaji ambazo hazikuwa sahihi kuanzia tarehe 3 hadi 7 Aprili, 2025.